Kujiunga na #GenerationRestoration: Kuboresha Mifumo ya Ekolojia kwa manufaa ya Watu, Mazingira na Hali ya Hewa hukusanya ushahidi kuhusu hali ya uharibifu wa mifumo ya ekolojia duniani na kutoa maelezo kuhusu manufaa kwa uchumi, kwa mazingira na kwa jamii yanayoweza kusababishwa na uboreshaji wa mifumo ya ekolojia. Ripoti hii inaonyesha kuwa, mbali na kuwa bora, uboreshaji wa mifumo ya ekolojia unahitajika kwa kiwango kikubwa ili kufikia ajenda ya maendeleo endelevu. Utumiaji wa malighafi kupindukia umejikita katika uchumi na mifumo ya utawala, na uharibifu unaosababishwa unadhoofisha mafanikio ya maendeleo yaliyopatikana kwa bidii na kutishia ustawi wa vizazi vijavyo.
Nchi zinahitaji kutimiza ahadi zake zilizopo za kurejesha hekta bilioni 1 za ardhi iliyoharibiwa na kutoa ahadi sawia kwa maeneo ya bahari na ya pwani. Uboreshaji wa mifumo ya ekolojia ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za kutoa masuluhisho kutokana na mazingira kushughulikia kutojitosheleza kwa chakula, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na uharibifu wa bayoanuai. Haitatokea kwa haraka wala kwa urahisi, na mabadiliko makubwa yanahitajika kuhusiana na tunavyopima kukua kwa uchumi hadi kwa jinsi tunavyopanda chakula na kile tunachokula. Lakini uzuri wa uboreshaji wa mifumo ya ekolojia ni kwamba unaweza kutokea kwa kiwango chochote - na kila mtu ana wajibu wa kutekeleza.