“COP28 imetoa, kwa mara ya kwanza katika mazungumzo ya mazingira, wito wa wazi kwa nchi kuachana na nishati ya visukuku. Mpango huu una dosari yake, lakini jambo moja liko wazi: ulimwengu hauendelei kukataa tuna mazoea mabaya ya kutumia nishati ya visukuku inayodhuru. Sasa hatutaongea tu bali tutachukua hatua. Kama alivyosema Katibu Mkuu, kuachana na nishati ya visukuku ni jambo lisiloweza kuepukika.
"Hii inamaanisha kuchukua hatua halisi za kuwa na mabadiliko ya haraka ya kuachana na nishati ya visukuku, hasa kwa nchi za G20, na hatua halisi kuhusiana na mambo mengi mazuri mengine yaliyofikiwa katika COP28: mfumo wa Lengo la Kimataifa la Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, uendelezaji wa Mfuko wa Hasara na Uharibifu, na ahadi mpya za kupunguza joto kwa njia endelevu, upunguzaji wa methani, kuimarisha mara tatu zaidi malengo ya nishati jadidifu na mafanikio ya mazingira.
"Ukweli, kama ilivyoainishwa katika ripoti ya UNEP ya Pengo la Uzalishaji wa Gesi Chafu liyotolewa kabla ya COP, ni kwamba hatuelekei kuwa na ulimwengu thabiti, wenye hewa kidogo ya ukaa na wa haki. Ukweli huu bado haujabadilika. Sasa kazi ngumu ya kuacha kuzalisha hewa ya ukaa ni sharti ianze.
"Ili kuwa na matumaini yoyote ya kufanya hivi kulingana na vile sayansi inavyotaka tufanye, ni sharti tutoe ufadhili zaidi ili kusaidia nchi katika kipindi cha mabadiliko ya haki, usawa na yasiochafua mazingira, ambacho ni muhimu sana kwa mataifa yanayoendelea ambayo lazima yakaze mwendo kupunguza hewa ya ukaa. Ufadhili na njia za utekelezaji kwa hivyo ni muhimu, kwa kuwa kila nchi inayoendelea lazima iwe na uwezo wa kumaliza haraka umaskini wa nishati, kufikia uwezo wake wa maendeleo endelevu na kutimiza SDGs.
“Tuna masuluhisho; tunajua ni nini kinachopaswa kufanywa. Na hatuwezi kusubiri tena kuchukua hatua."