Nairobi, Julai 23, 2024 – Huku kiwango cha joto na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi zinapoendelea kuathiri mabilioni ya watu kote duniani, Umoja wa Mataifa na washirika wake wametangaza mfululizo wa mikutano ya kikanda inayolenga kuongeza ahadi katika awamu inayofuata ya ahadi za tabia chini ya Mkataba wa Paris.
Katika mwaka wa 2025, nchi zinatakiwa kuwasilisha Mikati Mipya ya Kitaifa ya Kushughulikia Tabianchi (NDCs). Mipango hii inajulikana kama NDCs 3.0. Katika NDC hizi, nchi zinahimizwa kuweka malengo makubwa kufikia mwaka wa 2035 ya kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa katika maeneo yote ya uchumi kwa njia inayooana na kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzijoto 1.5 na kuimarisha ustahimilifu dhidi ya athari za tabianchi.
"Ili kutoa haki ya tabianchi kwa wote na kuhifadhi sayari inayowezesha maisha, uzalishaji wa gesi ya ukaa ni lazima upungue kwa kiasi kikubwa na juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinapaswa kuimarishwa," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP). "Hata hivyo, uzalishaji wa gesi ya ukaa haupungui, joto duniani linazidi kuongezeka na watu walio hatarini zaidi wanateseka. NDCs 3.0 lazima zilingane na nyakati tunazokabiliana nazo na kuwa bora zaidi."
Ili kuzisaidia nchi kuunda ahadi zake za tabianchi za awamu inayofuata chini ya Mkataba wa Paris, UNEP, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ushirikiano wa NDC kwa ushirikiano na Sekretarieti ya UNFCCC (Shirika la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi), wanaandaa Mikutano ya Kikanda ya NDCs 3.0.
"Wahusika wamekubaliana kuhusu utaratibu wa kukabiliana na hali hiyo chini ya Mkataba wa Paris kwa sababu ni chombo muhimu cha kutumiwa kupimia hatua na wanatambua umuhimu wa kuendelea kuwa makini tunapokabiliwa na mabadiliko ya tabianchi," alisema Simon Stiell, Katibu Mtendaji wa Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi. "Hatuwezi kuendelea kutopiga hatua: kuwasilisha Mikakati Mipya ya Kitaifa sio muhimu tu kwa kutimiza mahitaji ya kuripoti, lakini pia ni muhimu kwa kulinda mustakabali wa sayari yetu kwa manufaa ya vizazi vijavyo. Mikutano ya Kikanda ya NDCs 3.0 itasaidia wahusika wote kutekeleza ahadi zao."
Ratiba ya Mikutano ya Kikanda ya NDCs 3.0 itakayofanyika katika mwaka wa 2024 ni kama ifuatavyo:
- Mkutano wa Eneo la Pasifiki, kuanzia tarehe 12 hadi 16 Agosti mwaka wa 2024 utaandaliwa na serikali ya Samoa mjini Apia.
- Mkutano wa Eneo la Amerika ya Latini na Karibiani, kuanzia tarehe 27 hadi 29 Agosti mwaka wa 2024 utaandaliwa na serikali ya Kolombia mjini Bogota.
- Mkutano wa Eneo la Ulaya Mashariki, kuanzia tarehe 3 hadi 5 Septemba utaandaliwa na serikali ya Uturuki mjini Istanbul
- Mkutano wa Eneo la Mashariki ya Kati na Kusini mwa Afrika, kuanzia tarehe 23 hadi 25 Septemba mwaka wa 2024 utaandaliwa nchini Tunisia mjini Tunis
- Mkutano wa Eneo la Asia, kuanzia tarehe 30 Septemba hadi tarehe 2 Oktoba mwaka wa 2024 utaandaliwa mjini Bangkok, nchini Thailand
- Mkutano wa Eneo la Afrika, kuanzia tarehe 7 hadi 9 Oktoba mwaka wa 2024 utaandaliwa na serikali ya Rwanda mjini Kigali
Mikutano hii itakuwa ya faragha, inayolenga maafisa wa serikali wanaoshughulikia upitiaji wa NDCs kutoka nchi zote katika kila eneo. Ushirikishwaji na uwakilishi sawa utazingatiwa kupitia mwaliko kwa wazungumzaji waliochaguliwa kutoka kwa vijana na vikundi vingine vyenye uwakilishi mdogo na waliotengwa.
Yanayohitaji kufikiwa na NDCs 3.0
Ripoti ya UNEP ya mwaka wa 2023 ya Pengo la Uzalishaji wa Hewa Chafu iligundua kuwa NDC zilizopo zinaweza kufanya ulimwengu kushuhudia ongezeko la joto la kati ya nyuzijoto 2.5 na 2.9. Ingawa uchafuzi unakadiriwa kutengemaa baada ya mwaka wa 2030, bado haupungui haraka vya kutosha kufikia malengo ya kisayansi kulingana na Ripoti ya Usanisi wa NDC ya mwaka wa 2023. Kuweza kufikia nyuzijoto 1.5, kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa duniani kwa asilimia 42 kunahitajika kufikia mwaka wa 2030.
Wakati uo huo, Ripoti ya UNEP ya mwaka wa 2023 ya Kukabiliana Na Pengo la Uzalishaji wa Gesi Chafu iligundua kuwa ufadhili wa kukabiliana na pengo ni dola za Marekani kati ya bilioni 194 na bilioni 366 kwa mwaka. Kukabiliana na hali kwa kutegemea nchi, kukiungwa mkono na fedha zinazofaa, vinahitajika kwa dharura.
Mikutano hii itatumia maarifa kutoka kwa COP28 na Tathmini ya Kimataifa kuangazia jinsi ya kukabiliana na hali, masuluhisho ya kukabiliana na hali na ujumuishaji wa vichafuzi vikuu vya hewa (vichafuzi vya muda mfupi visivyo vya CO2), kama vile methani na kaboni nyeusi katika NDCs.
Washiriki, walioalikwa kutoka wizara za serikali zinazojishughulisha na ukuzaji na utekelezaji wa NDC, watashiriki katika kupata mafunzo kutoka kwa wenzao, kuangazia miundo bunifu ya ufadhili na kushiriki jinsi ya kuunda ramani za sera zitakazoongoza utekelezaji. Mikutano hii itatumiwa kujadili jinsi shabaha kabambe za kisekta zinavyoweza kupelekea mabadiliko na mipango ya uwekezaji.
Mabadiliko ya tabianchi pia ni kichocheo kikuu cha uharibifu wa mazingira na bayoanuai, huku uharibifu wa mazingira ukiwa kichochezi kikuu cha mabadiliko ya tabianchi. Vyanzo mabadiliko ya tabianchi mara nyingi ni sawa na vyanzo vya uchafuzi wa mazingira na taka, kwa hivyo majanga haya yana uhusiano na masuluhisho yanapaswa kuunganishwa.
Kisha mikutano hii itahimiza nchi kuzingatia manufaa kushughulikia mazingira na kutoa mifano ya jinsi ya kuoanisha shabaha za tabianchi na ahadi nyingine za kimataifa kuhusu asili, uchafuzi wa mazingira na maendeleo endelevu katika NDC zao.
Mikutano ya Kikanda ya NDCs 3.0 itaandaliwa kwa ushirikiano na washirika wengine, ikiwa ni pamoja na Muungano wa Mazingira na Hewa Safi (CCAC) unaongozwa na UNEP, Mpango wa REDD wa Umoja wa Mataifa, na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), pamoja na wabia wa kikanda wanaojumuisha Sekretarieti ya Mpango wa Mazingira wa Kanda ya Asia (SPREP), Kamisheni ya Kiuchumi na Kijamii ya Asia na Pasifiki (ESCAP), na Kamisheni ya Kiuchumi na Kijamii ya Asia Magharibi (ESCWA) ya Umoja wa Mataifa, na Benki ya Maendeleo ya Asia.
Makala kwa Wahariri
Nukuu za ziada
UNDP
"Mwaka wa 2024 na wa 2025 ni fursa bora kwetu kama jamii ya kimataifa kuhakikisha kuwa ongezeko la joto halizidi nyuzi 1.5, na kuzuia athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi. Umoja wa Mataifa unahamasisha mfumo wetu mzima na washirika wetu kusaidia nchi zinazoendelea kufikia lengo hili thabiti kupitia mpango wa UNDP wa Ahadi kwa Mazingira -- na Mikutano ya Kikanda ya NDCs 3.0 yatakuwa muhimu kupimia hali ya joto duniani kwa sasa ilipo na kubainisha fursa mpya za kubadilisha mustakabali wa hali ya hewa ulimwenguni”, alisisitiza Msimamizi wa UNDP, Achim Steiner.
Ushirikiano wa NDC
"Mikutano ya Kikanda ya NDC 3.0 inatokea wakati muhimu kufuatia Tathmini ya kwanza ya Kimataifa, na kuzileta pamoja serikali za nchi zinazoendelea ili kutafakari na kujadili kuhusu fursa za malengo ya NDC ambazo zina athari kubwa na zinafaa katika ngazi ya kitaifa. Kuongezeka ahadi, zilizojumuishwa katika serikali nzima na kujumuisha jamii nzima, kutachochea utekelezaji wa haraka wa mipango, sera na mikakati, na kusaidia kupata fedha kwa kiwango kikubwa", alisema Pablo Vieira, Mkurugenzi wa Kimataifa, Ushirikiano wa NDC.
Waziri wa Mazingira na Maendeleo Endelevu wa Kolombia
Kama Kolombia, tunaamini sana kwamba mikutano hii ni jukwaa la kimkakati na mwafaka la kuongoza ujumuishaji wa ajenda za bayoanuai na ajenda katika eneo letu. Tunapoelekea COP ya Mkataba wa Uanuai wa Kibayolojia (CBD) na COP 29 ya Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), mkutano huu utakuwa muhimu kuzingatia uwezekano wa malengo ya kikanda au maeneo ambayo yatashiriki shwa katika michakato ya kimataifa kuhusiana na mada hizi mbili muhimu. Matukio haya yanawakilisha fursa adhimu ya kuendeleza juhudi zetu kuongeza ahadi za kushughulikia mazingira na utekelezaji bora wa NDCs, yote chini ya kaulimbiu kuu ya "Amani na Mazingira." Zaidi ya hayo, tunasisitiza nia yetu tena ya kukuza ushirikiano na kuweka wazi njia za kuelezana na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuzuia hasara na uharibifu, na kukuza kanuni za amani, haki za binadamu na mbinu nyingine mtambuka kama vile jinsia, vizazi, haki ya mazingira, na kujumuisha makabila, vijijini na maeneo mbalimbali”, alisema Mheshimiwa María Susana Muhamad González, Waziri wa Mazingira na Maendeleo Endelevu wa Kolombia.
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira anayeweka ajenda ya kimataifa ya mazingira, huwezesha utekelezaji thabiti wa vipengele vya maendeleo endelevu ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, na kufanya kazi kama mtetezi mkuu wa maswala ya mazingira aliye na mamlaka.
Kuhusu Sekretarieti ya UNFCCC:
Sekretarieti ya UNFCCC (Shirika la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi) ni taasisi ya Umoja wa Mataifa iliyo na mamlaka ya kushughulikia tishio la mabadiliko ya tabianchi. Mkataba huu una wanachama kutoka karibu pembe zote za dunia na ni mkataba uliozaa Mkataba wa Paris wa mwaka wa 2015. Lengo kuu la UNFCCC ni kupunguza viwango vya gesi ya ukaa angani kwa kiwango ambacho kitazuia kuingiliwa vibaya na binadamu na mfumo wa hali ya hewa.
Kuhusu Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
UNDP ni shirika kuu la Umoja wa Mataifa linalopigania kukomesha ukosefu wa haki wa umaskini, ukosefu wa usawa na mabadiliko ya tabianchi. Kwa kufanya kazi na mtandao wetu mpana wa wataalam na washirika katika nchi 170, huwa tunasaidia mataifa kukuza masuluhisho yaliyoingiliana na ya kudumu kwa watu na sayari.
Kuhusu Ushirikiano wa NDC:
Ushirikiano wa NDC ni muungano wa kimataifa, unaoleta pamoja zaidi ya wanachama 200, ikiwa ni pamoja na zaidi ya nchi 120, zilizoendelea na zinazoendelea, na takribani taasisi 100 kutekeleza hatua kabambe za kushughulikia mazingira ambazo zinasaidia kufikia Mkataba wa Paris na kuendeleza maendeleo endelevu.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:
Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa