Jamii ya wanasayansi haijawahi kupatana zaidi au kukubaliana zaidi kuhusu hitaji la mabadiliko ya kimataifa ya dharura ya kuwezesha matumizi endelevu ya rasilimali. Toleo hili la mwaka wa 2024 la Mtazamo wa Rasilimali Ulimwenguni linaonyesha umuhimu wa rasilimali kwa utekelezaji bora wa Ajenda 2030 na makubaliano ya kimataifa ya mazingira ya kukabiliana na changamoto za aina tatu duniani. Ripoti hii inaleta pamoja data bora zaidi iliopo, uwakilishaji na tathmini ili kuchanganua mienendo, athari kwa ujumla na athari kuzingatia makundi mbalimbali. Inaundwa kutokana na kazi ya zaidi ya miaka 15 ya kazi ya Jopo la Kimataifa la Ralimali, ikijumuisha tathmini za kisayansi na maoni kutoka kwa nchi, mtandao mkubwa wa washikadau katika nyanja hii na wataalam wa kikanda.
Ripoti hii inaonyesha jinsi, tangu toleo la mwaka wa 2019 la ripoti hii, mwenendo wa matumizi ya rasilimali duniani umeendelea kuongezeka au kuharakishwa. Ripoti hi pia inaonyesha jinsi mahitaji ya rasilimali yanavyotarajiwa kuendelea kuongezeka katika miongo ijayo. Hii ina maana kwamba, bila hatua za dharura na za pamoja, kufikia mwaka wa 2060 uchimbaji wa rasilimali unaweza kuongezeka kwa asilimia 60 kwa kuzingatia viwango vya mwaka wa 2020 – na kusababisha kuongezeka kwa uharibifu na vitishio.
Hata hivyo, mambo hayapaswi kusalia hivi. Ripoti hii pia inaelezea uwezekano wa kugeuza mienendo mibovu na kuwezesha binadamu kuanza kuishi kwa njia endelevu.
Kwa hivyo, hatua thabiti za kisera ni muhimu ili kuachana na shughuli zisizo endelevu, kuharakisha njia za kuwajibika na bunifu za kukidhi mahitaji ya binadamu na kuunda hali mwafaka inayokubalika kwa jamii na usawa katika mabadiliko muhimu. Hii ni pamoja na hatua za haraka za kujumuisha rasilimali katika uwasilishaji wa mikataba ya kimataifa ya mazingira, kuweka njia za matumizi endelevu ya rasilimali na kuzindua mipango mwafaka ya kutia motisha ya kifedha, kibiashara na kiuchumi. Uwezekano wa kufikia uendelevu unazidi kuwa finyu na kukabiliwa na changamoto, na fursa iliopo inadidimia. Sayansi iko wazi: Swali kuu sio tena ikiwa mabadiliko ya utumiaji na uzalishaji wa rasilimali kwa njia endelevu ni muhimu, lakini jinsi ya kufanya hili lijiri sasa. Kushughulikia ukweli huu, kwa msingi wa dhana zinazobadilika za mabadiliko ya haki, ni sehemu muhimu ya mbinu yoyote inayoaminika na inayokubalika ya kutuwezesha kusonga mbele.