Yepi ni mapya kwenye hii ripoti
Ripoti ya Uzalishaji wa Gesi Chafu ya Mwaka wa 2021 inaonyesha kuwa ahadi mpya za mazingira zikijumuishwa na mikakati mingineyoya kushughulikia mazingira inaonyesha ulimwengu unaenda kushuhudia ongezeko la joto la nyuzijoto 2.7 kufikia mwisho wa karne hii. Hiki ni kinyume cha malengo la Mkataba wa Paris kuhusu mazingira na itapelekea mabadiliko mabaya mno kwa mazingira Duniani. Ili kufaulu kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzijoto 1.5 katika karne hii, kama inavyojitokeza kwenye malengo ya Mkataba wa Paris, dunia inahitaji kupunguza nusu ya uzalishaji wa gesi chafu kwa kipindi cha miaka nane ijayo.
Zikitekelezwa kikamilifu, ahadi za kutozalisha gesi chafu zinaweza kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 2.2, kiwango karibu na nyuzijoto 2 kilicho kwenye malengo ya Mkataba wa Paris. Hata hivyo, nyingi ya mipango ya kitaifa ya kushughulikia mazingira itaanza kushughulikiwa baada ya mwaka wa 2030.
Kupunguza uzalishaji wa methani kutoka kwa mafuta ya visukuku, taka na sekta za kilimo kunaweza kuchangia kupunguza pengo la uzalishaji wa gesi chafu na kupunguza ongezeko la joto kwa kipindi kifupi.
Masoko ya kaboni pia yanaweza kusaidia kupunguza uzalishaji wa gesi chafu. Lakini haya yatatokea tu iwapo sheria zitafafanuliwa wazi na zilenge upunguzaji halisi wa uzalishaji wa gesi chafu, na huku zikiungwa mkono na mipango ya kufuatilia maendeleo kwa njia ya uwazi.