Mambo mapya katika ripoti ya mwaka huu
Ripoti hii ni toleo la 13 katika mfululizo wa ripoti ya kila mwaka inayotoa muhtasari wa tofauti kati ya hali ya uzalishaji wa hewa chafu unavyotarajiwa kuwa katika mwaka wa 2030 na inavyopaswa kuwa ili kuzuia athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi.
Ripoti inaonyesha kwamba ahadi zilizosasishwa za kitaifa tangu kutokea kwa COP26 - iliyofanyika mwaka wa 2021 mjini Glasgow, Uingereza - zinapelekea mabadiliko machache ikilinganishwa na makadirio ya mwaka wa 2030 ya uzalishaji wa hewa chafu na kwamba tungali mbali kufika lengo la Mkataba wa Paris la kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzijoto 2, au ikiwezekana nyuzijoto 1.5. Utekelezaji wa sera zilizopo kwa sasa utapunguza tu ongezeko la joto hadi kati na nuzijoto 2.4 na 2.6 kufikia mwisho wa karne hii, kwa ahadi zinazotolewa kwa hiari na zile zinazotolewa kwa masharti mtawalia.
Ripoti hiyo inabaini kuwa ni mabadiliko ya haraka ya mfumo mzima tu ndiyo yanayoweza kudhibiti uzalishaji wa hewa chafu unaohitajika kufikia mwaka wa 2030: Asilimia 45 ikilinganishwa na makadirio kwa kuzingatia sera zilizopo kwa sasa ili kuwezesha kufikia nyuzijoto 1.5 na asilimia 30 kufikia nyuzijoto2. Ripoti hii inaangazia kwa undani jinsi ya kuleta mabadiliko haya, kwa kuangazia hatua zinazohitajika katika sekta ya usambazaji wa umeme, viwanda, uchukuzi na ujenzi, na mifumo ya chakula na fedha.