Hotuba iliyoandaliwa kuwasilishwa katika mkutano wa waandishi wa habari kuzindua Muhtasari kwa Watungasera wa Kikundi Kazi I kuchangia Ripoti ya 6 ya Tathmini ya Jopo la Serikali Mbalimbali kuhusiana na Mabadiliko ya Tabianchi inayojulikana kama “Mabadiliko ya Tabianchi 2021: Msingi wa Sayansi Halisi.”
Abdalah Mokssit, Katibu, Jopo la Serikali Mbalimbali kuhusiana na Mabadiliko ya Tabianchi
Petteri Taalas, Katibu Mkuu, Shirika la Hali ya Hewa Duniani
Dkt Hoesung Lee, Mwenyekiti, Jopo la Serikali Mbalimbali kuhusiana na Mabadiliko ya Tabianchi
Natoa shukrani kwa Jopo la Serikali Mbalimbali kuhusiana na Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), waandishi na kila mtu aliyeshiriki kuzungumzia suala la mabadiliko ya tabianchi. Kazi yenu inavutia tukizingatia usumbufu uliosababishwa na COVID-19.
Mmekuwa mkitufahamisha kwa zaidi ya miongo mitatu kuhusu hatari za kuruhusu ongezeko la joto duniani. Dunia iliwasikiliza, ila haikuwasikia. Dunia iliwasikiliza, ila haikuchukua hatua dhabiti. Matokeo yake ni changamoto ya mabadiliko ya tabianchi tunayoshuhudia kwa sasa. Hakuna aliye salama. Na hali inazidi kuwa mbaya zaidi kwa kasi.
Ni sharti tuchukulie suala la mabadiliko ya tabianchi kama tishio linalopaswa kushughulikiwa kwa dharura, jinsi tunavyopaswa kushughulikia changamoto zinazoingiliana za uharibifu wa mazingira, uharibifu wa bioanayoanuai, na uchafuzi na taka kwa dharura. Kama ilivyobainishwa hivi karibuni na IPCC na Jukwa la Kimataifa la Sayansi la Kuhudumia Bayoanuai na Mifumo ya Ekolojia (IPBES), mabadiliko ya tabianchi huzidisha hali mbaya dhidi ya bayoanuai na makaazi asilia na yanayodhibitiwa. Uharibifu wa mifumo ya ekolojia huharibu uwezo wa mazingira kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Na kama inavyotukumbusha ripoti ya IPCC ya Kikundi Kazi I, kupunguza gesi ya ukaa hakutapunguza tu kasi ya mabadiliko ya tabianchi, bali kutaboresha ubora wa hewa. Ni mambo yanayoingiliana.
Ni wakati wa kushughulika kwa sababu kila uzalishaji wa tani moja ya CO2 unasababisha ongezeko la joto duniani. Kama UNFCCC ilivyobaini wiki iliyopita, ni washirika 110 tu kati ya 191 Wanachama wa Mkataba waliowasilisha NDCs mpya au zilizosasishwa kabla ya COP ijayo ya tabianchi. Serikali zinapaswa kuweka mikakati ya kutozalisha gesi ya ukaa kama sehemu muhimu ya ahadi zao za mkataba wa Paris. Lazima zifadhili na kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kama ilivyoahidiwa katika Mkataba wa Paris. Zinapaswa kusitisha uzalishaji wa gesi ya ukaa upesi. Zirejeshe mifumo ya kiasili inayopunguza kaboni. Zipunguze gesi ya methani na gezi nyinginezo za ukaa. Zikamilishe kutekeleza mabadiliko ya Kigali yalifanyiwa Protokali ya Montreal kupunguza athari za viwanda vya kupunguza joto kwa mazingira. Na kila shirika la biashara, kila mwekezaji, kila raia wanapaswa kutekeleza wajibu wao.
Hatuwezi kuzuia yalitokea awali. Lakini kizazi hiki cha viongozi wa kisiasa na mashirika makuu ya biashara, kizazi hiki cha raia walio na uelewa, kinaweza kurekebisha mambo. Kizazi hiki kinaweza kufanya mabadiliko ya kimfumo yatakayozuia ongezeko la joto duniani, kusaidia kila mtu kukabiliana na hali mpya na kuunda ulimwengu ulio na amani, ustawi na usawa.
mabadiliko ya tabianchi yapo sasa. Na sisi pia tupo kwa sasa. Na tusipochukua hatua, ni nani atakayezichukua.
Asanteni.
Mkurugenzi Mtendaji