Iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji Inger Andersen.
Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) linaonyesha mshikamano na mabilioni ya watu kutoka pembe zote za dunia wanaokabiliwa na athari zinazotokana na COVID-19.
Tunatoa shukran zetu za dhati kwa mamilioni ya wahudumu wa afya na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) wanaofanya kazi bila kuchoka ili kutulinda tunapokabiliana na janga kubwa kuwahi kutokea katika historia tangu wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Suala nyeti wakati huu ni kuwalinda watu kwa kuzuia wasiambukizwe na COVID-19. Tunatambua kuwa virusi hivi vinapaswa kushughulikiwa ipasavyo, ndiposa tuko tayari kushirikiana na Nchi Wanachama na wabia wakuu wa Umoja wa Mataifa kwa kutoa ushauri wa kiufundi kuhusu ushughulikiaji wa kemikali na taka hatari wanapotafuta kukabiliana na taka inayoongezeka kutokana na ukabilianaji wa janga hili katika sekta ya matibabu.
Licha ya sheria ya kudhibiti mzunguko wa watu katika nchi ambazo UNEP hufanya kazi, UNEP inaendelea "kufanya kazi" huku ikiendelea kufuata sheria zote zinazowekwa na serikali na WHO. Kama UNEP, tunaendelea kufanya kazi yetu ya kudumisha utunzaji wa mazingira kote ulimwenguni kwa kupitia mtandao kuendeleza mijadala mingi inayohusiana na mazingira. Hii ni kutokana na ukweli kuwa afya ya watu na mazingira mazuri ni vitu vinavyotegemeana.
Matendo ya binadamu yameathiri sayari yetu yote, kuanzia kwa ardhi hadi kwa bahari. Na tunapoendelea kuathiri mazingira na hudhoofisha mifumo ya ekkolojia, tunahatarisha maisha ya binadamu. Kwa kweli, asilimia sabini na tano ya magonjwa yote ambukizi huzuka kutoka kwa wanyama. Inamaanisha kuwa virusi hutoka kwa mifugo au wanyamapori hadi kwa wanadamu.
UNEP inashirikiana na wabia wanaofanya utafiti wa kisayansi kuonyesha uhusiano uliopo kati ya mifumo dhabiti ya ekolojia, mazingira na afya ya binadamu ikijumuisha magonjwa kutoka kwa wanyama.
Ni kutokana na uhusiano kati ya viumbe vyote duniani ndiposa kuna umuhimu wa kuweka mikakati ya kushughulikia bayoanuai hadi baada ya mwaka wa 2020. Nasi tunaendelea kuhakikisha kuwa hili litafikiwa.
Na katika mazingira ya baada ya janga wakati serikali zinapoidhinisha mambo yatakayowezesha kubuniwa kwa nafasi za kazi, kupunguza umaskini, kukuza na kuimarisha uchumi, tutaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama na wabia "kujiimarisha", kubuni fursa za kutumia nishati isiyochafua mazingira, kama vile nishati jadidifu, nyumba za kisasa, kuwezesha umma kununua bidhaa zisizochafua mazingira na magari yasiyochafua mazingira. Haya yote yanaongozwa na kanuni na sheria za uzalishaji na matumizi ya bidhaa kwa njia endelevu.
Hatua hizi, —ushughulikiaji mwafaka wa taka hatari zinazotokana na huduma za matibabu na kemikali; na kujitolea "kujiimarisha", kubuni nafasi za kazi zisizochafua mazingira na kuleta mabadiliko kwa kutozalisha gesi ya ukaa katika siku zijazo ni muhimu iwapo tunataka kuwa na hatima endelevu iliyo dhabiti na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu. Na hiyo ndiyo hatima tunayoitaka bila shaka.