Nairobi, Septemba 7, 2021 - Uchunguzi mpya wa kimataifa wa sera na programu za kuboresha hali ya hewa unaonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita nchi zaidi zimepitisha sera kuhusu sekta zote kuu zinazochafua mazingira. Ila upungufu mkubwa katika utekelezaji, ufadhili, uwezo, pamoja na ufuatiliaji, inamaanisha kuwa viwango vya uchafuzi wa hewa vinasalia kuwa juu. Data hii imechapishwa leo, Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na angaa za bluu, katika ripoti mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).
Ripoti hiyo, Juhudi kuhusu ubora wa hewa: muhtasari wa sera na programu za kupunguza uchafuzi wa hewa duniani, inatokatokana na data ya utafiti wa hivi karibuni kutoka nchi 195. Inakagua sera na programu katika sekta kuu zinazochangia uchafuzi wa hewa: uchukuzi, uzalishaji wa nishati, uzalishaji wa gesi chafu viwandani, usimamizi wa taka mango, uchafuzi wa hewa nyumbani, na kilimo. Pia inaangazia ufuatiliaji wa ubora wa hewa, usimamizi wa ubora wa hewa na viwango vya ubora wa hewa kama vifaa muhimu kisera vya kupunguza athari za uchafuzi wa hewa.
Kuanzia mwaka wa 2020, nchi 124 (takribani theluthi mbili) ziligunduliwa kuwa na viwango bora vya kitaifa vya ubora wa hewa, nchi 17 zaidi ya ilivyoripotiwa katika mwaka wa 2016. Lakini, ni asilimia 9 tu ya nchi hizi zinazingatia viwango viliviyowekwa na miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Ripoti hiyo inaonesha kuwa ingawa nchi zenye kipato cha chini huathiriwa zaidi kutokana na uchafuzi wa hewa, hatua za kupunguza uchafuzi wa hewa zina manufaa mengi kwa maendeleo, ikijumuisha kupunguza mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha mazao ya kilimo, usalama wa nishati, na ukuaji wa uchumi.
Inger Andersen, Katibu Mtendaji wa UNEP, alisema: “Serikali zinapozinapochukua hatua kuboresah hali ya hewa, husaidia kuzuia vifo vya mapema vya watu milioni saba kila mwaka. Pia huboresha afya kwa jumla wa na uchumi wa asilimia 92 ya idadi ya watu ulimwenguni wanaoishi mahali ambapo viwango vya ubora wa hewa vimezidi mipaka ya Shirika la Afya Duniani (WHO). Leo, tuna sera nyingi zaidi kuliko hapo awali, lakini ni muhimu kabisa tuzingatie utekelezaji, haswa pale ambapo watu wameathiriwa sana na hali mbaya ya hewa.”
Tangu mwaka wa 2016, wakati UNEP ilipoanza kufuatilia hatua za serikali kuhusu ubora wa hewa, kumekuwa na uboreshaji kutoka kwa uzalishaji wa gesi chafu viwandani, uchukuzi, usimamizi wa taka mango, na uchafuzi wa hewa nyumbani. Kwa mara ya kwanza, ripoti pia inachuguza sera na programu zilizopo za kilimo, usimamizi na viwango vya hali ya hewa:
- Tangu mwaka wa 2016, nchi 18 zaidi zimeongeza viwango vipya vya uzalishaji wa gesi chafu wa magari sawa na Yuro 4/IV au zaidi, na kufanya idadi jumla kufikia nchi 71. Licha ya nchi nyingi za kipato cha chini kuendelea kutokuwa na sheria kuhusu viwango vya uzalishaji wa magari yaliyotumika kutoka nje ya nchi, idadi kubwa ya sheria za kitaifa zinajitokeza kupunguza miaka ya magari yaliyoingizwa na kuhamasisha raia kujikwamua na magari ya zamani yanayochafua mazingira. Kwa mfano, Moroko inaruhusu tu uagizaji wa magari chini ya miaka mitano na yanaofikia viwango vya uzalishaji wa gesi chafu vya magari vya EURO4; kwa hivyo, inapokea tu magari ya hali ya juu na yale yaliyotumiwa yasiyochafua mazingira kutoka Uropa, kwa kuzingatia mapendekezo ya UNEP;
- Nchi 21 zaidi zimepitisha sera za uzalishaji usiochafua mazingira na kufanya idadi jumla kufikia nchi 108;
- Nchi 95 zina programu zinazoendeleza upikaji na upashaji joto usiochafua mazingira, zikiwa na nchi mpya 13 ikilinganishwa na mwaka wa 2016. Hii imepunguza viwango vya magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa hewa majumbani, haswa Kusini na Mashariki mwa Asia na Pasifiki;
- Ingawa ni hali inayoendelea kushuhudiwa, nchi zaidi 26 sasa zinadhibiti kabisa uchomaji wa taka mango na kufanya idadi jumla kufikia nchi 38), ikijumuisha kuteka gesi takani, ukusanyaji ulioimarika, kutenga taka na njia mwafaka za utupaji taka;
- Nchi 58 zina mikakati ya kukuza kilimo endelevu, na kutumia njia mwafaka kupunguza uzalishaji wa methani, ikijumuisha njia mbadala kwa uchomaji wa mabaki ya kilimo, usimamizi bora wa mbolea ya mifugo, kutengeneza mbolea ili kupunguza taka ya chakula, na kutumia methani iliyotekwa kuunda nishati;
- Hata hivyo kati ya nchi 124 zilizo na viwango vya ubora wa hewa, ni 57 tu zinazofuatilia ubora wa hewa mara kwa mara, huku nchi 104 zikiwa hazina miundomsingi ya ufuatiliaji. Hii inaonesha mapungufu ya data yaliyopo na maswala ya uwezo ambayo hudhibiti upatikanaji wa ubora wa hewa duniani.
Licha ya sera mpya za hewa safi katika nchi kote ulimwenguni na kushuka kwa kasi kwa gharama za magonjwa kutokana na uchafuzi wa hewa majumbani katika baadhi ya maeneo, takwimu za afya zinaonyesha kuwa uchafuzi wa hewa majumbani na nje unasalia kuwa hatari kuu kwa afya duniani. Kuboresha hali ya hewa, kutahitaji kutekelezwa vizuri kwa sera na sheria zilizopo, ufadhili mkubwa zaidi, na ufuatiliaji ulioenea zaidi na uwezo dhabiti.
UNEP inatoa wito kwa nchi kujumuisha uwekezaji katika kushughulikia uchafuzi wa hewa katika mipango yake ya kujiimarisha baada ya COVID-19. Inaomba pia kuweka vigezo vya kutathmini hatua za sasa na za baadaye za kuwa na hewa safi na kuondoa vizuizi katika utekelezaji wa sera na programu, ikijumuisha ufadhili na upungufu wa uwezo, na kukabiliana na changamoto za gharama na utunzaji wa vifaa vya ufuatiliaji.
Juhudi kuhusu ubora wa hewa: muhtasari wa sera na programu za kupunguza uchafuzi wa hewa duniani, inakamilishana na mihtasari za ripoti sita za kikanda (kutoka Afrika, Asia na Pasifiki, Ulaya, Amerika ya Latini na Karibiani, Amerika ya Kaskazini, na Asia Magharibi, ni ripoti inayoonesha juhudi kupitia matendo za sekta kuu, pamoja na mienendo kikanda na viapumbele. UNEP itakuza matokeo ya ripoti hii na itaendelea kutumia maoni kutoka kwa nchi wanachama kufuatilia maendeleo ya hatua za kuboresha hali ya hewa na kuelimisha ili kushughulikia mapungufu na changamoto ulimwenguni.
MAKALA KWA WAHARIRI
Kuhusu Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu
Likisisitiza umuhimu wa kufanya juhudi zaidi za kuboresha hali ya hewa, ikijumuisha kupunguza uchafuzi wa hewa, kutunza afya ya binadamu; kukiri kuwa kuboresha hali ya hewa kunaweza kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinaweza kuboresha hali ya hewa; Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliamua kuteua tarehe 7 Septemba kama Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu.
Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)
UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni. UNEP Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Keisha Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa,