Uchafuzi wa hewa umerejelewa kama hatari kubwa zaidi kwa afya nyakati zetu, na husababisha vifo vya mapema vya takribani watu milioni 7 kila mwaka. Takribani watu tisa kati ya 10 kote ulimwenguni huvuta hewa chafu, hali inayopelekea uwezekano wa kukumbwa na pumu, ugonjwa wa moyo na saratani ya mapafu.
Wanaoishi mijini, hasa watu maskini, mara nyingi huathiriwa vibaya zaidi na uchafuzi wa hewa, ambao mbali na kudhuru afya huchochea mabadiliko ya tabianchi. Kwa kutambua hatari hizo, manispaa nyingi zinachukua hatua za kukabiliana na vichafuzi wa hewa.
Tunapoelekea Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu tarehe 7 Septemba, hafla ya kila mwaka inayosisitiza umuhimu wa kuimarisha hali ya hewa kwa dharura, tunaangalia miji mitano kati ya hiyo.
Bogota, Colombia
Bogota ni mojawapo wa nchi zilizo mstari mbele Amerika ya Kusini kupunguza uchafuzi wa hewa. Jiji linatumia umeme kwa mtandao wake wa mabasi ya umma na linalenga kutumia umeme kabisa kwenye mfumo wake wa metro, sehemu ya mpango kabambe wa kupunguza uchafuzi wake wa hewa kwa asilimia 10 kufikia mwaka wa 2024. Meya wa Bogota, Claudia López Hernández, pia ameangazia umuhimu wa baiskeli.
"Sasa tuna zaidi ya safari milioni 1 za baiskeli kila siku," alisema katika mwaka wa 2020. Ingawa uchafuzi mwingi wa Bogotá unatokana na usafiri, mioto misituni katika maeneo na nchi jirani pia imeongezea hali hiyo.
Warsaw, Poland
Poland ni nyumbani kwa miji 36 kati ya 50 ya Jumuiya ya Ulaya iliyochafuliwa zaidi, huku uchafuzi wa hewa ukisababisha vifo vya mapema 47,500 kila mwaka. Sasa inakabiliana na hali hii, baada ya kutia saini Azimio la C40 la Miji ya Hewa Safi katika mwaka wa 2019. Mapema mwaka huu, ilizindua Breathe Warsaw, ushirikiano na Mfuko wa Hewa Safi na Bloomberg Philanthropies ili kuboresha hali ya hewa. Warsaw sasa ina vihisi hewa 165 kote jijini, mtandao mkubwa zaidi barani Ulaya, na Breathe Warsaw itavitumia kutengeneza hifadhidata ya ubora wa hewa, na kuruhusu maafisa kuelewa vyema vyanzo vya uchafuzi. Mpango huu pia utatoa usaidizi wa kiufundi ili kusaidia hatua ya kuondolewa kwa upashaji joto wa makaa ya mawe, kuweka eneo la uzalishaji mdogo wa hewa chafu kufikia mwaka wa 2024 na kuunganisha viongozi wa eneo hilo kushiriki mbinu bora zaidi.
Seoul, Korea Kusini
Huku kukiwa na watu milioni 26 wanaoishi katika Greater Seoul, haishangazi kuwa jiji hilo linakabiliwa na janga la ubora wa hewa. Hakika, wastani wa kukumbana kwa Wakorea na chembe hatari inayojulikana kama PM2.5 ni ya juu zaidi kuliki jimbo lolote katika Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo. Viwango vya PM2.5 katika Seoul ni karibu mara mbili zaidi ya vile vya miji mikuu katika nchi zilizoendelea. Katika mwaka wa 2020, jiji hili lilitangaza kuwa litapiga marufuku magari ya dizeli kutoka kwa sekta zote za umma na meli za usafiri wa umma kufikia mwaka wa 2025. Wakati uo huo, ushirikiano na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) utachunguza mafunzo yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita kuhusu uboreshaji wa hali ya hewa na kusaidia kushiriki uzoefu huu na miji mingine katika eneo hili.
Accra, Ghana
Accra ulikuwa mji wa kwanza kujiunga na kampeni ya BreatheLife na inachukuliwa kuwa mstari mbele kati ya miji barani Afrika inayolenga kukabiliana na uchafuzi wa hewa. Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu 28,000 hufa mapema kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa, huku viwango wastani vya uchafuzi wa hewa katika mji mkuu wa Ghana vikiwa mara tano kuliko miongozo ya WHO. Jiji hili limeanza kampeni ya kuelimisha watu juu ya hatari za kiafya za majiko ya ndani ya nyumba na kuwazuia wenyeji kuchoma taka zao. Juhudi za pamoja kati ya WHO na Muungano wa Mazingira na Hewa Safi zinasaidia kutathmini katika jiji zima manufaa ya kiafya ya kuanza kutumia mifumo endelevu zaidi ya nishati kwa uchukuzi, taka nyumbani.
Bangkok, Thailand
Kwa kuzingatia msongamano wa magari, Bangkok ni mojawapo ya baadhi ya misongamano mibaya zaidi duniani, haishangazi kwamba jiji hili mara nyingi hufanya kazi chini ya mzunguko wa uchafuzi. Katika mwaka wa 2020, mamia ya shule zililazimishwa kufungwa kwani viwango vya chembechembe laini - au PM2.5 - hewani vilifikia viwango visivyo salama. Jiji hili limezindua mipango kadhaa ya kukabiliana na uchafuzi wa hewa na uzalishaji wa hewa ya ukaa. Mradi wa Green Bangkok 2030, uliozinduliwa katika mwaka wa 2019, unalenga kuongeza nafasi ya kijani jijini hadi mitamraba (sqm) 10 kwa kila mtu, kufanya miti kukalia asilimia 30 ya eneo lote la jiji, na kuhakikisha njia za miguu zinakidhi viwango vya kimataifa. Bustani kumi na moja zimepangwa kufunguliwa wakati wa awamu ya kwanza ya mradi huu, pamoja na barabara inayopakana na miti ya kilomita 15, zote zikiwa na lengo la kuwezesha utegemezi mdogo kwa usafiri wa kibinafsi, na hivyo kupunguza uchafuzi.
Kulingana na ripoti ya UNEP ya mwaka wa 2021 ya Hatua za Kushughulikia Ubora wa Hewa, nchi zinazidi kutumia motisha au sera zinazohimiza uzalishaji kwa njia isiyochafua mazingira, matumizi mazuri ya nishati na upunguzaji wa uchafuzi wa viwanda na kuwa na sera zaidi zinazoharamisha uchomaji taka mango. Lakini, mengi zaidi yanahitaji kufanywa. Ni asilimia 31 tu ya nchi zina mifumo ya kisheria ya kudhibiti au kushughulikia uchafuzi wa hewa unaovuka mipaka, huku asilimia 43 ya nchi zikiwa hazina ufafanuzi wa kisheria wa uchafuzi wa hewa. Nchi nyingi bado hazina mifumo thabiti ya ufuatiliaji wa ubora wa hewa na ya usimamizi wa ubora wa hewa.
Ukosefu wa usawa pia ni sababu ya uchafuzi wa hewa, huku zaidi ya asilimia 90 ya vifo vinavyotokana na uchafuzi wa hewa hutokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati, hasa barani Afrika na Asia. Hata ndani ya miji, maeneo maskini yanaathiriwa zaidi na uchafuzi wa hewa kuliko maeneo tajiri.
Kila mwaka, tarehe 7 Septemba, ulimwengu huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu. Siku hii inalenga kuhamasisha na kuwezesha kuchukuliwa kwa hatua za kuimarisha ubora wa hewa. Ni wito kwa jamii ya kimataifa kutafuta njia mpya za kufanya mambo, kupunguza kiwango cha uchafuzi wa hewa tunachosababisha, na kuhakikisha kwamba kila mtu, popote alipo anaweza kufurahia haki yake ya kuvuta hewa safi. Kaulimbiu maadhimisho ya tatu ya kila mwaka ya Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi ili kuwa na anga za bluu, yalioendeshwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, ni “Hewa Tunayovuta pamoja.”