Ni yepi mapya katika ripoti ya mwaka huu?
Ripoti hii inaangazia mikakati, ufadhili, na utekelezaji wa juhudi za kukabiliana na hali. Angalau asilimia 84 ya Wanachama wa Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) wamejumuisha mipango, mikakati, sheria, na sera – ongezeko la asilimia 5 ikilinganishwa na mwaka jana. Inaendelea kuwa bora zaidi na kutoa kipaumbele kwa makundi yanayotengwa kama vile watu wa kiasili.
Hata hivyo, ufadhili wa kuwezesha kutekeleza mipango na mikakati hii hautoshi. Ufadhili wa kimataifa wa kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na hali bado ungali chini kati ya mara 5 na 10 kwa kuzingatia mahitaji yaliyokadiriwa kuziba pengo linaloongezeka. Makadirio ya mahitaji ya kila mwaka ya kukabiliana na hali ni dola za Marekani kati ya bilioni 160 na bilioni 340 kufikia mwaka wa 2030 na dola za Marekani kati ya bilioni 315 na bilioni 565 kufikia mwaka wa 2050.
Utekelezaji wa hatua za kukabiliana na hali – uliojikita katika kilimo, maji, mifumo ya ekolojia na sekta anuai – unaimarika. Hata hivyo, bila kuimarisha ufadhili, hatua za kukabiliana na hali zinaweza kuzidiwa na madhara yanayoongeza ya mabadiliko ya tabianchi, hali itakayopelekea kupanuka kwa pengo la kukabiliana na hali.
Ripoti hii inazungumzia manufaa ya kutoa kipaumbele kwa juhudi za kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa na kusaidia jamii kukabiliana na hali, kama vile masuluhisho kutokana na mazingira na kutoa wito kwa nchi kuimarisha ufadhili na utekelezaji wa hatua za kukabiliana na hali. Kwa kuongezea,ripoti hii inajadili kuhusu ufanisi wa kukabiliana na hali na kuonyesha uhusiano kati ya juhudi za kudhibiti na kukabiliana na hali pamoja na manufaa ya kushirikiana.